Bahari ya Amundsen ni mkono wa Bahari ya Kusini upande wa magharibi wa Bara la Antaktiki kwenye eneo la longitudo ya 110°[1]. Upande wa mashariki inapakana na Bahari ya Bellingshausen, upande wa magharibi hakuna sehemu ya bahari iliyopewa jina maalumu, hadi Bahari ya Ross kwa umbali wa km 1,000.[2]
Bahari imefunikwa na barafu kwa muda mrefu wa mwaka. Barafuto inayosukuma barafu baharini ina unene wa kilomita 3 na eneo lake ni kilomita za mraba 700,000.
Bahari hiyo imepewa jina lake kwa heshima ya Roald Amundsen, mpelelezi wa ncha za Dunia kutoka nchini Norwei, aliyekuwa binadamu wa kwanza aliyefaulu kufika kwenye ncha ya kusini. Kwa miaka mingi mstari wa pwani haukujulikana kwa sababu unene wa barafu hauonyeshi tofauti kati ya bahari na nchi kavu. Tangu mwaka 1940 Mwamerika Richard Evelyn Byrd alifanya utafiti kwa msaada wa eropleni akaweza kutambua pwani.