Bahari ya Norwei ni bahari ya pembeni ya Atlantiki iliyopo upande wa kaskazini magharibi ya Norwei. Inapatikana baina ya Bahari ya Kaskazini na Bahari ya Greenland. Inaunganishwa na Bahari Atlantiki upande wa magharibi na upande wa mashariki kaskazini iko Bahari ya Barents.[1][2]
Kina cha Bahari ya Norwei ni kirefu, kwa wastani kilomita 2. Chini yake kuna akiba za mafuta ya petroli na gesi asilia ambazo Norwei imefaidi tangu mwaka 1993.
Kabla ya kugunduliwa kwa gesi asilia matumizi ya kiuchumi ya bahari hii yalikuwa hasa ya uvuvi. Pwani za Bahari ya Norwei huwa na samaki wengi wanaofika huko kuzaa kutoka Atlantiki ya Kaskazini. [3] Lakini idadi ya samaki imepungua kutokana kwa kuzidi kwa uvuvi unaotumia vifaa vya kisasa.[4]
Mkondo wa Atlantiki ya Kaskazini hufikisha maji vuguvugu yasiyoweza kupoa mno, hivyo sehemu hii ya bahari haiwezi kuganda hata wakati wa baridi.