Balozi ni mwakilishi rasmi wa serikali ya nchi yake katika nchi nyingine. Anatumwa huko na wizara ya mambo ya nje akitazamwa kama mwakilishi wa mkuu wa nchi inayomtuma.
Kwa kawaida anaongoza ofisi ya ubalozi ambako anasaidiwa na wanadiplomasia wengine wanaotumwa katika utaratibu wa diplomasia.
Nchi zinazopokea ubalozi zinakubali pia kinga ya kidiplomasia inayomaanisha ya kwamba balozi na wanadiplomasia wenzake hawawezi kukamatwa wala kuadhibiwa katika nchi wanapotumwa kwa kosa lolote. Vilevile majengo ya ubalozi hutazamwa kama ardhi ya nchi nyingine ambako polisi ya nchi ulipo haiwezi kuingia. Mzigo wake haiwezi kufunguliwa na maafisa wa forodha au polisi katika nchi alikotumwa. Utaratibu huu ulikubaliwa katika Mkataba wa Vienna juu ya Mahusiano ya Kidiplomasia wa 1961.
Balozi mpya anatumwa na barua rasmi kutoka wizara yake akikubaliwa na nchi anapohudumia. Nchi inayompokea inaweza kumwambia pia aondoke tena.
Balozi hutumwa kwenda nchi nyingine kwa miaka kadhaa akirudi baadaye katika nchi yake ambako anaweza kuendelea kufanya kazi ndani ya wizara au kutumwa tena kwa nchi nyingine.