Benki ni taasisi inayoshughulika biashara ya fedha. Shughuli zake za msingi ni pamoja na kukopa na kukopesha fedha.
Kwenye ngazi hii benki inatunza pesa ya watu wengi. Kwa utunzaji huu benki haiachi pesa kukaa bure tu lakini inaitumia kwa biashara yake. Inaitumia kukopesha kampuni au watu wanaohitaji fedha.
Wanaokopa pesa wanalipa riba ambayo ni mapato ya benki kwa huduma ya kukopesha; kutokana na mapato haya benki inalipa pia riba ndogo zaidi kwa wale waliopeleka pesa zao kwake. Tofauti kati ya viwango vya aina hizi mbili za riba ni faida na pato la benki. Jambo muhimu linaloangaliwa na benki wakati wa kukopesha pesa ni uwezo wa mkopaji kurudisha deni lake.
Asili ya benki ilikuwa biashara ya wakopeshaji fedha. Siku hizi kuna benki za aina mbalimbali pamoja na:
Benki za biashara ambazo ni makampuni yanayolenga kupata faida kubwa kwa kutoa huduma za kifedha. Benki hizi zinashughulikia mawasiliano kati ya watu au makampuni yenye pesa za ziada na watu au makampuni wanaohitaji pesa.
Benki za ushirika ambazo mara nyingi hazilengi faida kubwa lakini huduma kwa wateja wasio na pesa nyingi; benki hizi zinapokea pia kiasi kidogo cha pesa na kutoa mikopo kwa wajengao nyumba au wafanyabiashara wadogo. Benki hizi hutumia mfumo wa uwekezaji pesa ili kujikuza pamoja na wateja wao. Wamarekani pia hutumia mbinu hii ambayo wanaiita 401k.
Benki kuu ambayo kwa kawaida ni taasisi ya serikali inayosimamia utoaji wa pesa taslimu na kiasi cha pesa inayopatikana sokoni kwa jumla. Inasimamia pia kazi ya benki za biashara na za ushirika.