Dola la Roma (kwa Kilatini "Imperium Romanum") lilikuwa milki kubwa lililoenea kwa karne kadhaa katika nchi zote zinazopakana na bahari ya Mediteranea (ambayo kwa sababu hiyo iliitwa "Mare Nostrum", yaani "Bahari yetu") na nyinginezo.
Lilianza kwenye mji mkuu wa Roma na rasi ya Italia ikaendelea kuunganisha makabila na mataifa ya nchi nyingi kwenye mabara matatu ya Ulaya, Afrika na Asia.
Kuanzia karne ya 1 KK Watawala wa Dola wakaitwa makaisari: Kaisari wa kwanza alikuwa Augusto.
Nchi nyingi za sasa ziliwahi kuwa sehemu ya Dola la Roma kama vile Uingereza, Ufaransa, Hispania, Italia, Ugiriki na nchi za Balkani upande wa Ulaya, Moroko, Algeria, Tunisia, Libia na Misri upande wa Afrika, na Uturuki, Syria, Lebanon, Palestina, Jordan na hata Irak upande wa Asia.
Idadi ya wakazi imekadiriwa kuwa ilifikia milioni 50-90, yaani asilimia 20 hivi za watu wote duniani wakati huo.
Lugha ya Dola la Roma ilikuwa Kilatini, ila katika sehemu za mashariki pamoja na Kigiriki cha Kale.
Sehemu ya magharibi ya Dola la Roma iliishia mwaka 476 baada ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Kaisari wa mwisho Romulus Augustulus aliyefukuzwa na jemadari wa Kigermanik wa jeshi la Roma.
Upande wa mashariki Dola la Roma likaendelea hadi mwaka 1453 kwa majina kama "Roma ya Mashariki" au Bizanti.