Elimu kwa maana pana ni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi. Katika dhana ya kiufundi, elimu ni njia ambayo hutumiwa makusudi na jamii kupitisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine.
Walimu katika taasisi za elimu huratibisha elimu ya wanafunzi wao kupitia masomo kama vile ya kuandika, kusoma, kuhesabu (hisabati), sayansi na historia. Mbinu hii wakati mwingine huitwa masomo haswa tunaporejelea somo la aina fulani, kwa kawaida mbinu hii hutumiwa na maprofesa katika taasisi za masomo ya juu.
Kuna elimu maalumu kwa wale wanaohitaji ujuzi wa kitaaluma, kama vile wanaohitaji kuwa marubani. Juu ya hayo, kuna nafasi nyingi za elimu katika viwango vingine visivyo rasmi kama vile majumba ya ukumbusho, maktaba pamoja na mtandao na tajriba za maisha.
Haki ya kusoma imeweza kuelezwa kuwa haki ya msingi ya binadamu katika kifungu cha pili cha itifaki ya kwanza ya maagano ya haki za binadamu barani Ulaya kuanzia mwaka wa 1952 ambapo wanachama wote wanashurutishwa kuhakikisha elimu kwa wote. Katika kiwango cha kimataifa, Mapatano ya Umoja wa Mataifa ya haki za kiuchumi, za kijamii na za kiutamaduni katika mwaka wa 1966 yanahakikisha haki hii katika kifungu cha 13.