Fasihi simulizi ni kazi ya sanaa inayotumia mdomo (tofauti na maandishi kama kwenye fasihi andishi) kama njia kuu ya kufikisha ujumbe. Ni sehemu ya msingi ya utamaduni na vipengele vyake vingi vinafanya kazi kama katika fasihi kwa jumla.
Katika jamii isiyo na uandishi ni wazi kuwa hakuna fasihi andishi. Hata hivyo kila jamii ina hazina ya mapokeo yapokelewayo Kwa mdomo na kihifadhiwa katika maandishi kwa mfano: utenzi, ngano au nyimbo za jadi. Hivyo vyote ni sehemu za fasihi simulizi.
Hata jamii ijuayo kusoma na kuandika inaendelea kuwa na fasihi simulizi, hasa nyumbani, k.m. katika kuwasimulia watoto hadithi. Lakini mara nyingi fasihi simulizi ya jamii ijuayo kusoma na kuandika ni tofauti sana na fasihi simulizi ya jamii isiyo na uandishi, kwa vile imeathiriwa na ujuzi wa kusoma na kuandika, na mitindo ya masimulizi yake hayaendi sambamba na mitindo ya masimulizi yasiyoathiriwa na uandishi.