Hali ya hewa (pia: halihewa) ni namna ya kutaja yale yanayotokea katika sehemu ya chini ya angahewa juu ya uso wa dunia katika eneo fulani na wakati fulani.
Hali hizi hutofautishwa kulingana na upepo, halijoto, mawingu, unyevuanga, kanieneo, mnururisho wa jua, uvukizaji na kadhalika.
Athari muhimu zaidi katika mabadiliko ya halihewa ni mzunguko wa angahewa unaotawaliwa na nishati ya mnururisho wa jua na uwiano wa kanieneo katika sehemu mbalimbali za angahewa.
Tabia muhimu za halihewa hutokea kama upepo, dhoruba, kimbunga, radi, mvua, theluji na baridi au joto zikiathiri maisha ya binadamu.
Hali ya hewa inaenda sambamba na tabianchi yaani, kama ni ya joto au baridi, bichi au yabisi. Mabadiliko ya hali ya hewa hurahisisha maisha au kuongeza ugumu wake, hasa kama mabadiliko yanavuruga kukua kwa mimea kwa njia ya ukame au mafuriko.
Watu hujenga makao na kuvaa nguo kulingana na halihewa na kwa njia hiyo tabianchi imekuwa nguvu ya kufinyanga utamaduni wa watu.