Kanisa maana yake ya kwanza kabisa ni "mkusanyiko wa waamini" kama ule wa Waisraeli chini ya Musa kwenye mlima Sinai walipopewa Amri za Mungu.
Neno hilohilo lilitumiwa na Wakristo wa kwanza kwa ajili yao wenyewe kusema wameshika nafasi ya Israeli kama taifa la Mungu hata wasipokuwa Wayahudi bali watu wa mataifa mengine.
Jina hilo lilitumika kwa jumuia mama ya Yerusalemu, kwa kila mojawapo ya jumuia za Kikristo zilizotokana na umisionari wa wafuasi wa Yesu Kristo, na kwa umoja wao wa kimataifa uliotazamwa na Mtume Paulo kuwa Mwili wa Kristo, ukiwa na Yesu kama kichwa chake. Ndiye anayesadikiwa kuwa chemchemi ya ukombozi wa wanadamu wote pale alipolifia Kanisa na kuliachia sakramenti kuu ya Pasaka (ekaristi takatifu).
Kanisa ni “Mkusanyiko” maana ndani yake Roho Mtakatifu anaunganisha na Yesu na kati yao wale waliopokea Neno la Mungu na sakramenti zake. “Bwana alilizidisha Kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa… Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja” (Mdo 2:47; 4:32). Ndio tokeo la ombi la Yesu: “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma” (Yoh 17:21). Kumbe utitiri wa madhehebu yaliyotenganika unaleta picha ya “mtawanyiko” ambayo inakwaza ulimwengu usisadiki. “Kila mtu wa kwenu husema, ‘Mimi ni wa Paulo’, na, ‘Mimi ni wa Apolo’, na, ‘Mimi ni wa Kefa’, na, ‘Mimi ni wa Kristo’. Je, Kristo amegawanyika?” (1Kor 1:12-13).
Kwa imani hiyo, Kanisa si kundi la binadamu tu, tunaloweza kulianzisha kama vile chama, timu n.k. Kanisa ni fumbo la Mwili wa Kristo unaohuishwa na Roho Mtakatifu. Kama Yesu linaonekana upande wa ubinadamu tu, kumbe linaunganisha utu na Umungu. Baba “alivitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa, ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote” (Ef 1:22-23).
Hivyo hatuwezi kuambatana na Yesu kwa kulikataa Kanisa, kwa kuwa hao wawili ni mwili mmoja, kama Bwanaarusi na Bibiarusi. “Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, ‘Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe” (Math 19:4-6). “Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa” (Ef 5:32).
Kwa sababu hiyo Kanisa ni muhimu kwa wote kwa kuwa ndilo ishara na chombo cha umoja wa watu na Mungu na kati yao. Yesu “aliwapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu. Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja” (Ef 2:16-18).