Kanisa Katoliki ni jina linalotumika kwa maana mbalimbali, lakini hasa kumaanisha Kanisa la Kikristo linalokubali mamlaka ya kiroho ya Papa wa Roma kama mkuu wa urika wa maaskofu juu yake lote.
Ndilo kubwa kabisa kati ya madhehebu yote ya dini hiyo, likikusanya nusu ya wafuasi wote wa Yesu.
Hata hivyo, Wakristo wa madhehebu mengine wanaokubali kanuni ya imani ya Nisea-Konstantinopoli wanatafsiri tofauti sehemu yake inayokiri Kanisa la kweli kutambulishwa na sifa nne, ya tatu ikiwa kwamba ni katoliki: "Tunasadiki Kanisa moja, takatifu, katoliki, la Mitume".
Kanisa Katoliki, likiwa na miaka karibu elfu mbili, ni kati ya miundo ya zamani zaidi iliyopo duniani na imechangia kwa kiasi kikubwa ustaarabu wa Magharibi, ingawa tangu mwishoni mwa Karne za Kati athari yake inazidi kupungua, ilivyo wazi leo hasa katika masuala yanayohusu jinsia na uzazi.
Imani ya Kanisa hilo inatokana na ufunuo wa Mungu ulivyotolewa kwa Israeli na ulivyokamilishwa na Yesu ambaye alimtambulisha kama Baba na alilianzisha kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetumwa naye juu ya Mitume wake siku ya Pentekoste mwaka 30 (au 33) BK.
Ni imani inayoungamwa katika ubatizo, sakramenti ya kwanza na mlango wa sakramenti nyingine sita: kwamba Mungu ni mmoja tu katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.
Imani hiyo inatakiwa kutekelezwa katika maadili maalumu yanayotegemea hasa upendo ambao ndio adili kuu na uhai wa mengine yote.
Kutokana na juhudi za kutekeleza matendo ya huruma kwa yeyote mwenye shida, Kanisa Katoliki linatoa huduma za elimu na afya kuliko taasisi nyingine yoyote duniani kote.
Kama vielelezo vya utakatifu ambao waamini wote wanaitiwa, Kanisa linapendekeza watu wa Agano la Kale na wa Agano Jipya, hasa Bikira Maria, lakini pia wale waliojitokeza zaidi katika historia yake kama watakatifu.
Baadhi yao wana wafuasi wengi wanaounda familia za kiroho, mara nyingi kama mashirika ya kitawa yenye karama mbalimbali.