Kanisa la Kilatini (wakati mwingine "Kanisa la Kiroma") ni moja ya madhehebu yanayounda Kanisa Katoliki. Ndiyo kubwa kuliko yote (97% za waumini wote), likiwa na Wakristo zaidi ya bilioni 1 duniani kote.
Mengine ni Makanisa Katoliki ya Mashariki (3%) yanayofuata mapokeo na hasa liturujia kama ya Waorthodoksi lakini yakiwa na ushirika kamili na Papa wa Roma ambaye ndiye mkuu wa Kanisa la Kilatini, pamoja na kwamba ni pia mkuu wa Kanisa Katoliki lote.
Jina linatokana na kwamba kwa karne nyingi lugha pekee iliyotumika katika ibada zake ilikuwa Kilatini.
Kanisa hilo lote upande wa sheria linafuata Mkusanyo wa sheria za Kanisa, kumbe upande wa liturujia wengi wa waamini wake wanafuata mapokeo ya Kanisa la Roma, lakini wengine wanafuata mapokeo ya Ambrosi wa Milano, au yale ya Lyon, Braga, Toledo na ya mashirika mbalimbali ya kitawa (k.mf. Wakartusi na Wadominiko).
Hivi karibuni waamini waliotokea madhehebu ya Anglikana wameruhusiwa kuendelea kutumia baadhi ya matini yake katika ibada wakiwa sasa ndani ya Kanisa la Kilatini.