Kiumbehai ni kitu chochote kilichoumbwa na kuwa na uhai, kama vile binadamu, mnyama, mmea au bakteria.
Kwa upande mmoja viumbehai ni molekuli za mata jinsi ilivyo kwa vitu vingine, kwa mfano udongo, mawe, fuwele au hewa. Kwa upande mwingine mata hii ina mfumo wenye tabia mbalimbali ambazo kwa pamoja zinaunda uhai kama vile uwezo wa kuzaa, kukua na umetaboli (uwezo wa kujenga au kuvunja kemikali mwilini).
Hata kama sayansi haijajua kikamilifu uhai ni nini inatambua jumla ya tabia hizo kama dalili za uhai.
Kiumbehai kinaweza kuwa na seli moja (kama bakteria kadhaa) au kuwa na seli milioni kadhaa kama mwanadamu.
Viumbehai vyenye seli moja tu ni vidogo sana: havionekani kwa jicho bali kwa hadubini tu.