Yesu kugeuka sura ni sikukuu ya liturujia ya Ukristo inayoadhimisha fumbo la maisha ya Yesu linalosimuliwa katika Agano Jipya[1], hususan katika Injili Ndugu (Math 17:1–9, Mk 9:2-8, Lk 9:28–36) na katika 2 Pet 1:16–18[1].
Humo tunasoma kwamba Yesu Kristo aliongozana na wanafunzi wake watatu, Mtume Petro, Yakobo Mkubwa na mdogo wake Mtume Yohane, hadi mlima kwa lengo la kusali faraghani.
Huko usiku alianza kung'aa akatokewa na Musa na Eliya waliozungumza naye kuhusu kufariki kwake Yerusalemu.
Kubwa zaidi, Mungu Baba alimshuhudia kuwa Mwana wake mpenzi akawahimiza wanafunzi hao kumsikiliza.[1]
Hivyo Wakristo wanaona tukio hilo kama dhihirisho la Mwana pekee wa Mungu, mpendwa wa Baba wa milele, lililokusudiwa kuonyesha hadi miisho ya dunia kwamba hali duni ya binadamu aliyoitwaa imekombolewa kwa neema na kwamba jinsi ilivyoumbwa kwa mfano wa Mungu, sasa imeumbwa upya katika Kristo baada ya uharibifu uliosababishwa na Adamu [2].
Tukio linaheshimiwa hasa na Ukristo wa Mashariki na wamonaki wanaoliona mwaliko wa kutazama utukufu wa Mungu uliofichama katika malimwengu, kumbe kwa sala unadhihirika kwa macho ya imani.
Fumbo hilo linaadhimishwa kila mwaka kama sikukuu tarehe 6 Agosti[3]. Pia linazingatiwa katika Rozari kama tendo la nne la mwanga.