Liturujia ya Antiokia, inayoitwa pia Liturujia ya Siria, ni jina la taratibu za ibada ya Wakristo ambayo ina asili yake katika mji wa Antiokia wa Siria (siku hizi umo katika mipaka ya Uturuki) ambao katika karne ya 1 ulikuwa kituo kikuu cha umisionari wa Kanisa, halafu ukawa na shule ya teolojia muhimu kama ile shindani ya Aleksandria (Misri).
Wanaotumia liturujia hiyo ni hasa Kanisa la Kiorthodoksi la Siria na madhehebu yenye uhusiano naye kihistoria (hasa matawi ya Kanisa la Kiorthodoksi la Kisiria la Malankara kutoka India), na yale yaliyotokana nalo, yakiwa pamoja na Kanisa Katoliki la Kisiria na Kanisa Katoliki la Kimalankara. Kwa kiasi kikubwa liturujia hiyo ni pia ya Kanisa la Wamaroni.