Maendeleo

Kwa matumizi tofauti ya jina hili angalia hapa Maendeleo (maana)

Nyumba bora ya kuishi Salinas, California, Marekani.

Maendeleo ni mabadiliko yanayoonekana kuboresha hali ya binadamu.

Hali hiyo inajitokeza katika nyanja mbalimbali za maisha na kulisha mawazo mengi.

Upande wa sayansi yanahusika na ongezeko la ujuzi kutokana na utafiti na mabadilishano ya matokeo yake.

Upande wa historia yanahusishwa na utambuzi wa kwamba ulimwengu unaweza kuboreshwa zaidi na zaidi kutokana na mchango wa sayansi, teknolojia, uhuru n.k.

Upande wa jamii yanahusishwa na tarajio la kwamba binadamu anaweza kupata hali bora zaidi na zaidi katika mafungamano, siasa, uchumi n.k.

Upande wa falsafa yanahusishwa na tumaini au hakika ya kuwa hali ya binadamu itazidi kuwa bora. Kinyume chake, wengine wanaonyesha kwamba vipindi vya ustawi vinafuatwa na vingine ambapo maendeleo hayatokei, sanasana ni kurudi nyuma.

Kwa jumla, ni muhimu kutambua kwamba si kila badiliko linaleta maendeleo, au walau maendeleo ya upande mmoja yanaweza yakaendana na hali yu kurudi nyuma upande mwingine.

Mara nyingi inatajwa teknolojia ambayo ikitumika vibaya inaweza kuharibu maadili, uchumi n.k. hata kuangamiza kabisa uhai (k.mf. mabomu ya nyuklia).

Itafaa daima kukumbuka kaulimbiu ya Julius K. Nyerere: "Maendeleo ni watu, si vitu". Wengine wanauliza, "Maendeleo ya watu ni yapi? Na maendeleo ya vitu ni yapi?"


Developed by StudentB