Mahakama ni mfumo wa wataalamu na kamati maalumu ambao unatafsiri na kutumia sheria katika jina la wananchi, la jamhuri au la mfalme.
Mahakama pia inatoa mfumo wa kutatua migogoro. Chini ya mfumo wa mgawanyo wa madaraka mahakama kwa ujumla haitungi wala haiundi sheria (ambayo ni kazi ya bunge) wala kutekeleza sheria (ambayo ni wajibu wa serikali), bali inatafsiri sheria na kutumia na kutekeleza katika ukweli wa kila kesi.
Mahakama ina kazi ya kuhakikisha usawa mbele ya sheria kwa watu wote.
Kwa kawaida kuna mahakama za ngazi mbalimbali; mahakama za juu zinapokea rufaa dhidi ya kesi za ngazi za chini hadi mahakama ya rufaa ya mwisho inayoitwa mahakama kuu au mahakama ya katiba. Tawi hili la mahakama lina uwezo wa kubatilisha sheria zisizolingana na katiba ya nchi.
Neno "mahakama" pia hutumika kumaanisha kwa pamoja maafisa ndani yake kama vile majaji, mahakimu na makarani wengine.