Mifano ya Yesu inaweza kusomwa katika Injili zote nne za Agano Jipya katika Biblia ya Kikristo, lakini pia katika Injili nyingine zilizoandikwa baadaye. Injili ya Luka ndiyo inayoongoza kwa wingi wa mifano (50 hivi).
Ni sehemu muhimu ya utume wa Yesu, ikiwa sawa na thuluthi moja ya mafundisho yake yote yaliyotufikia kwa maandishi.
Wakristo wanatia maanani sana mifano hiyo kama maneno ya Yesu yanayohitaji kufikiriwa zaidi ili kuelewa yanataka kusema nini kweli.[1][2]
Ni kwamba mifano ya Yesu inaonekana kwanza hadithi za kuvutia zinazochora vizuri maisha ya watu yalivyokuwa katika mazingira yake. Hata hivyo wataalamu wanaonyesha kwamba ujumbe wa dhati umefichika hasa katika sehemu ya mwisho ya habari, ambapo kuna jambo lisilo la kawaida, yaani lisilotokea kweli.[3][4]
Ingawa mifano inaonekana kusimulia habari za kawaida, lengo ni kufikisha ujumbe wa kidini kwa wasikilizaji wenye nia njema, ambao wanapokea changamoto ya Yesu, "Mwenye masikio, na asikie!".
Mifano ya Yesu inabaki kati ya masimulizi maarufu zaidi duniani kote.[5]
Kwa Kiebrania neno husika ni מָשָׁל mashal linalodokeza pia fumbo au kitendawili. Agano la Kale lilikuwa tayari na mifano ya namna hiyo, hivyo Wayahudi wa wakati wa Yesu waliweza kuelewa ya kwake kwa urahisi fulani.[6]