Mkoa wa Dar es Salaam ni kati ya mikoa 31 ya Tanzania. Umepakana na Mkoa wa Pwani pande zote barani na Bahari ya Hindi upande wa mashariki.
Eneo la mkoa ni jiji la Dar es Salaam ambalo ndilo kitovu cha shughuli za biashara (na za utawala, kwa kiasi fulani) nchini Tanzania, na ni kati ya majiji yanayokua haraka zaidi duniani.
Ni km² 1,800 pamoja na visiwa vidogo 8 na eneo la bahari kati ya pwani na visiwa hivyo. Eneo la nchi kavu pekee ni km² 1,393.
Kuna wilaya tano: City (wakazi 1,649,912), Kinondoni (wakazi 982,328), Temeke (wakazi 1,346,674), Kigamboni (wakazi 317,902) na Ubungo (wakazi 1,086,912). Kila moja inaangaliwa kama mji. Takwimu hizo ni za sensa ya mwaka 2022, ambapo kwa jumla idadi ya wakazi ilikuwa 5,383,728 [1].
Wakazi asili wa eneo la mkoa ni Wazaramo ingawa kwa sasa kutokana na kukua na kupanuka kwa jiji, kuna makabila yote ya Tanzania, mbali ya wageni wengi kutoka nchi mbalimbali.