Mungu ni jina lenye asili ya Kibantu linalotumika kwa yeyote anayesadikiwa katika dini mbalimbali kuwa na uhai wa hali ya juu.
Kati ya wafuasi wa dini hizo, wengi wanaona kuwa Umungu, kwa jinsi ulivyo au unavyofirika, haukubali mgawanyiko. Hasa katika Uyahudi, Ukristo na Uislamu wanasisitiza umoja wa Mungu kuwa ndio msingi wa imani yao. Kwao Mungu ni wa milele, anafahamu yote na kutaka hasa uwepo wa viumbe. Tena kwa hiari yake alipenda kujifunua kwa binadamu; kielelezo ni Ibrahimu/Abrahamu aliyefanywa rafiki yake na baba wa waamini wote.
Kuna dini nyingine zinazokubali kuwepo kwa miungu mbalimbali (wawili au zaidi). Hasa dini nyingi za jadi zinaamini wingi wa miungu. Dini kubwa duniani inayosadiki miungu mingi ni Uhindu. Pia katika sehemu za Afrika ya Magharibi ibada za miungu mingi zinaendelea hadi leo.