Mwenyezi Mungu katika lugha ya Kiswahili ni jina linalotumika kwa Muumba wa kila kitu, Mwenye kuabudiwa kwa haki, kinyume na neno mungu ambalo linamaanisha chochote au yeyote anayeabudiwa ikiwa kwa haki au si kwa haki.
Neno Mwenyezi linaunganisha Mwenye na enzi na kumpatia Mungu sifa ya kuweza yote, bila kuzuiliwa na yeyote wala chochote.
Kwa uweza huo, Mwenyezi Mungu ni Muumba wa mbingu na dunia na kila kilichomo ndani yake, naye ni Mlezi wa viumbe vyote na Mpaji riziki kwa kila chenye uhai ulimwenguni.
Mwenyezi Mungu, katika dini na mila nyingi duniani, ni yule anayestahiki kuabudiwa kwa haki ikiwa peke yake bila kushirikishwa na chochote, au kwa kushirikishwa na viumbe, kwa nia ya kuwa hawa viumbe vinamkurubisha naye.
Hii ni kwa sababu, kila dini au mila ina namna yake ya kumsawiri Mwenyezi Mungu, na njia gani sahihi ya kumuabudu, na kwa kuwa hakuna itifaki baina ya hizi dini, mila na madhehebu kuhusu Mwenyezi Mungu na namna anavyotakikana kuabudiwa, hizi tofauti chungu nzima zimetokea.