Sarafu (kar. صرافة badilisha) ni kipande cha metali iliyotolewa na serikali ya nchi kama namna ya pesa. Mara nyingi sarafu ina umbo la duara kama kisahani. Kuna pia sarafu za pembe tatu, pembe nne au pembe zaidi.
Zamani sarafu ilikuwa umbo la kawaida ya pesa. Sarafu za kwanza zinazojulikana dunia zimepatikana kutoka Lydia katika Anatolia ya Magharibi iliyokuwa wakati ule sehemu ya utamaduni wa Wagiriki wa Kale. Sarafu zilitengenezwa hasa kwa kutumia metali ya thamani kama dhahabu na fedha, pia ya shaba na wakati mwingine ya chuma. Thamani ya sarafu ililingana na kiasi fulani cha metali hizi.
Siku hizi sehemu kubwa ya fedha inatolewa kama noti yaani kama karatasi. Karibu popote duniani sarafu hutumika kwa ajili ya pesa ndogo tu. Isipokuwa sarafu za dhahabu zinatolewa kwa idadi ndogo hasa kwa ajili ya watu wanaopenda kukusanya aina mbalimbali za sarafu zenye thamani ingawa hazitumiki kama pesa ya kulipia.