Uainishaji wa kisayansi (ing. biological classification, taxonomy) ni jinsi wataalamu wa biolojia wanavyopanga viumbehai kama mimea na wanyama kwa vikundi kwenye ngazi mbalimbali. Inaweza kuitwa pia taksonomia.
Tangu muda mrefu watu walitambua ya kwamba wanyama au mimea mbalimbali wanafanana kati yao kwa namna moja au nyingine. Wataalamu walijaribu kupanga aina hizo kwa vikundi vyenye tabia za pamoja. Carolus Linnaeus alianza kuzipanga kwa muundo ulioeleweka kulingana na tabia za maumbile yao.
Mfumo wa Linnaeus uliendelezwa baadaye kulingana na nadharia ya Charles Darwin inayoona ya kwamba spishi mbalimbali huwa na chanzo cha pamoja, kwa hiyo inawezekana kupanga uhai wote kama mti yenye matawi makubwa, tena madogo yanayotoka kwenye makubwa.
Ujuzi wa kisasa kutokana na utafiti wa DNA ndani ya seli za viumbehai unaendelea kuongeza ujuzi wetu kwa hiyo katika mengi uainishaji ni utaalamu unaozidi kubadilika.