Uchapaji ni njia ya kunakili maandishi na picha kwa karatasi au loho bapa nyingine, hata kitambaa.
Vitabu na magazeti vinatengenezwa kwa njia ya uchapaji. Hivyo vinaweza kutolewa kirahisi kwa nakala nyingi.
Kabla ya kupatikana kwa uchapaji vitabu, hati na maandiko yote yalinakiliwa kwa mkono pekee. Katika tamaduni mbalimbali waandishi na wanakili walikuwa mabingwa muhimu. Lakini kunakili matini ndefu kama kitabu kulichukua muda mrefu, hata miaka, hivyo vitabu havikupatikana kwa nakala nyingi, pia vilikuwa ghali mno.
Tangu kubuniwa kwa uchapaji maandishi yamepatikana kwa wingi tena kwa bei nafuu. Hii ilisaidia uenezaji wa habari na elimu na kusababisha mapinduzi makuu katika historia ya binadamu.[1][2][3][4]