Kuhusu nyota angalia hapa Mchoraji (kundinyota)
Uchoraji ni sanaa ya kuweka alama au picha kwa kutumia vifaa mbalimbali vya kuchorea, kama vile kalamu ya wino au ya risasi, burashi, penseli za rangi ya nta, crayoni, makaa, choko, pastels, aina mbalimbali za erasers, markers, styluses, metali mbalimbali (kama silverpoint) na siku hizi hata elektroniki au kitu kingine cha kuandikia au kupaka rangi katika karatasi, kitambaa, ubao, metali, mwamba, kadi, plastiki, ngozi, canvas, na bodi au penginepo.
Michoro ya muda mfupi inaweza kufanywa katika ubao mweusi au mweupe.
Tokeo la uchoraji huitwa mchoro au picha. Mara nyingine picha huchorwa kwa ustadi mkubwa sana.
Upatikanaji mpana wa vyombo vya kuchora hufanya uchoraji kuwa moja ya shughuli za kawaida za kisanii. Ni sanaa wakilishi maana inaweza kutumika kuwasilisha ujumbe kwa jamii, hivyo imekuwa njia maarufu na ya msingi ya kujieleza kwa umma katika historia ya binadamu. Ni njia rahisi na yenye ufanisi zaidi ya kuwasiliana mawazo ya kuona.
Mbali na namna zake zaidi za kisanii, kuchora mara nyingi hutumiwa katika biashara, usanifu, uhandisi na ufundi. Msanii anayeshughulikia au anafanya kazi katika kuchora kiufundi anaweza kuitwa pia mchoraji.
Hata hivyo kuna aina tofauti za uchoraji. Hii inategemea mchoraji mwenyewe anapenda aina gani ya uchoraji: wakati mwingine sanaa hii ya uchoraji si ya kuwakilisha ujumbe tu, bali pia kumvutia mtazamaji kwa rangi za kupendeza bila kujali ujumbe uliobebwa na picha hiyo. Wakati mwingine inawezekana picha isiwe na ujumbe kabisa, lakini ikawa imechorwa kwa ustadi mkubwa na kupakwa rangi za kuvutia sana, mpaka mtazamaji kumvutia na kumfanya apende kuendelea kuitazama picha husika.