Ufufuko wa Yesu ndio tukio kuu lililotangazwa daima na Kanisa lake lote kuhusu mwanzilishi wake, Yesu Kristo, kuanzia ushuhuda wa Mitume wa Yesu na maandiko ya Agano Jipya, hususan Injili, hadi leo.
Kadiri ya imani hiyo, siku ya tatu baada ya kuuawa msalabani Ijumaa kuu, Yesu alifufuka mtukufu akiacha kaburi lake na vitambaa vyote vilivyotumika kumzikia.
Tangu Jumapili hiyo na kwa muda wa siku arubaini (kadiri ya Matendo ya Mitume 1:3), yeye aliendelea kuwatokea mara kadhaa wanafunzi wake, hadi alipoonekana nao akipaa mbinguni huku akiwabariki.
Tukio hilo linaadhimishwa kila mwaka kwenye Pasaka ya Kikristo na kila wiki kwenye Dominika.
Kwa Wakristo, ufufuko wa Yesu ndiyo sababu na kielelezo cha ufufuko wa waadilifu wote siku ya kiyama.