Ukristo (kutoka neno la Kigiriki Χριστός, Khristos, ambalo linatafsiri lile la Kiebrania מָשִׁיחַ, Māšîăḥ, linalomaanisha "Mpakwamafuta" [1]) ni dini inayomwamini Mungu pekee[2] kama alivyofunuliwa kwa Waisraeli katika historia ya wokovu ya Agano la Kale na hasa Yesu Kristo katika Agano Jipya ambaye ni mwanzilishi wake katika karne ya 1.
Dini hiyo, iliyotokana na ile ya Wayahudi, inalenga kuenea kwa binadamu wote, na kwa sasa ni kubwa kuliko zote duniani,[3][4][5] ikiwa na wafuasi 2,400,000,000 (33% kati ya watu 7.274 bilioni)[6][7][8][9], ambao nusu ni waamini wa Kanisa Katoliki na nusu ya pili wamegawanyika kati ya Waorthodoksi (11.9%) na Waprotestanti (38%) wa madhehebu mengi sana.
Karibu wote wanakubali Utatu Mtakatifu, yaani kwamba milele yote Mungu ni nafsi tatu zenye umoja kamili: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Ni kwa jina lao kwamba mataifa yote wanahimizwa kubatizwa kwa maji, ili kuzaliwa upya, kadiri ya agizo la Yesu ili kuingizwa katika fumbo la Mungu pekee kupitia fumbo la kifo na ufufuko wake mwenyewe.
Kitabu kitakatifu cha Ukristo kinajulikana kama Biblia. Ndani yake inategemea hasa Injili na vitabu vingine vya Agano Jipya.
Wakati wa Mababu wa Kanisa misingi ya imani ya Ukristo ilifafanuliwa na Mitaguso ya kiekumeni namna inayokubaliwa na wengi kabisa kati ya Wakristo wa leo. Maungamo yao yanakiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu aliyefanyika mtu ili kuwaokoa binadamu. Baada ya kuteswa na kuuawa msalabani alizikwa ila akafufuka, siku ya tatu akapaa kwa Mungu akishiriki mamlaka ya Baba hadi atakaporudi kuhukumu waadilifu na wasiotubu, akiwapa tuzo au adhabu ya milele kadiri ya imani na matendo yao.
Hivyo, kati ya madhehebu ya Ukristo, karibu yote yanamkiri Yesu kuwa kwa pamoja Mungu kweli na mtu kweli: katika umoja na nafsi yake ya Kimungu zinapatikana sasa hali hizo zote mbili.
Yote yanamkiri kuwa Mwokozi wa watu wote, na kuwa ndiye atakayerudi mwishoni mwa dunia kwa hukumu ya wote, ingawa maelezo kuhusu jambo hilo yanatofautiana.
Vilevile yote yanamchukua kama kielelezo cha utakatifu ambacho - kwa msaada wa Roho Mtakatifu na wa sakramenti zilizowekwa na Yesu mwenyewe, kuanzia ile ya ubatizo - kiwaongoze ndani ya Kanisa katika maadili yao maalumu, kuanzia unyenyekevu na upole hadi upendo unaowaenea wote, bila kumbagua yeyote, hata adui.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link)
{{cite web}}
: Unknown parameter |=
ignored (help)
{{cite web}}
: Unknown parameter |=
ignored (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
{{cite web}}
: Unknown parameter |=
ignored (help)
{{cite web}}
: Unknown parameter |dead-url=
ignored (|url-status=
suggested) (help)