Ushirika kamili ni msamiati wa teolojia ya Ukristo kuhusu Kanisa.
Unamaanisha umoja kamili kati ya madhehebu mbalimbali kwa msingi wa imani ileile inayoyawezesha kushirikiana kikamilifu katika ibada na hasa ekaristi na sakramenti nyingine.[1]
Unatumika na Kanisa Katoliki, Waorthodoksi na Waorthodoksi wa mashariki, ukitofautishwa na ushirika usio kamili au wa kiasi tofautitofauti uliopo kati ya Wakristo wa aina zote kadiri wanavyozidi kusadiki mambo yaleyale ya msingi zaidi (kama vile Utatu mtakatifu, umungu wa Yesu Kristo na ufufuko wake), ingawa wanapishana katika mengine (hasa Kanisa na sakramenti).
Dhana ya ushirika kamili hutumiwa pia kutaja uhusiano baina ya makanisa ya Jumuiya Anglikana na pia kati ya makanisa mengine ya Kiprotestanti ambayo yameamua kutambuana na kushirikiana moja kwa moja.