Utume wa Yesu katika Injili, unaanza na ubatizo wake kwa mkono wa Yohane Mbatizaji katika mto Yordani na unakamilika katika mji mtakatifu wa Yerusalemu kwa kifo chake msalabani.[1]
Injili ya Luka (3:23) inasema Yesu Kristo alipoanza utume wake alikuwa "na umri wa miaka 30 hivi".[2]
Kwa kawaida wataalamu wa Biblia wanakadiria kwamba mwaka wa kubatizwa ulikuwa kati ya 27 na 29 BK na ule wa kuuawa kati ya 30 na 33.[3]
Awali Yesu, baada ya kubatizwa na kukaa siku 40 katika jangwa la Yudea, alifanya kazi ya kitume zaidi katika mkoa wa Galilaya, huko alikokulia,[4] akihubiri na kuponya, pamoja na kufukuza pepo wachafu.
Mbali ya hiyo miujiza yake, ni muhimu mwenendo wake wa kukaribiana na watu wa kila aina, bila ubaguzi: tendo lake la kushiriki karamu pamoja na wakosefu lilichukiza wengi, hasa kati ya madhehebu ya Mafarisayo waliokwepa watu hao. Kumbe kwa Yesu lilikuwa dokezo la kwamba Mungu anawaalika wote kutubu na kuingia raha ya ufalme wake.
Wakati huohuo aliita baadhi kumfuata kama wanafunzi katika safari zake. Kati yao aliteua mitume 12 kama mwanzo wa Kanisa lake.[1][5]Hao aliwaita mitume kwa sababu aliwapeleka kwanza kwa Waisraeli (Math 8) lakini baada ya kufufuka kwa mataifa yote pia (Math 28:16-20).[6][7]
Baada ya kifodini cha Yohane Mbatizaji, Yesu alijiandaa kwenda Yerusalemu kwa mara ya mwisho ili kukamilisha utume wake kwa kujitoa kafara alivyotabiriwa na Yohane: "Huyu ndiye mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu".[8][9]
Safari hiyo ya mwisho ilimchukua tena kwa muda karibu na mahali alipobatizwa.[10][11][12][13][14]
Utume wake wa mwisho mjini Yerusalemu ulianza na tukio la kuingia Yerusalemu kwa shangwe ya Wayahudi walioamini kwamba ndiye Masiya, hasa baada ya muujiza mkuu alioufanya, yaani kumfufua Lazaro wa Bethania kutoka kaburini siku ya nne baada ya kifo. Injili zinasimulia kirefu zaidi habari za hiyo wiki ya mwisho kutokana na umuhimu wake kama kilele cha yote.[15]