Waabbasi (Kar. العبّاسيّون al-‘abbasiyun) ni jina la nasaba ya makhalifa waliotawala milki kubwa ya Kiislamu kati ya 750 hadi 1258 BK. Mfululizo huo ulianzishwa na wajukuu wa Abbas ibn Abd al-Muttalib aliyekuwa mjomba wa Mtume Muhammad.
Mji mkuu wa Waabbasi ulikuwa Baghdad.
Waabbasi walichukua nafasi ya Wamuawiya waliokuwa nasaba ya kwanza wa makhalifa baada ya makhalifa wanne wa kwanza.
Khalifa wa kwanza Mwabbasi alikuwa Abu al-'Abbas as-Saffah aliyemshinda Marwan II na kutumia cheo cha khalifa. Al Mansur aliyemfuata alipeleka mji mkuu kwenda Baghdad.
Milki ilistawi kwa zaidi ya karne mbili. Baadaye watawala wa Bghdad walipaswa kukabidhi sehemu kubwa ya madaraka kwa watawala wadogo wa maeneo chini yao. Waturuki waliofika Baghdad kama wanajeshi wa ulinzi wa khalifa walipata polepole nafasi kubwa katika utawala wa milki. Khalifa ikawa cheo cha heshima kubwa lakini bila madaraka mengi.
Mashambulio ya Wamongolia yalivunja yale yaliobaki. Mwaka 1258 jemadari Hulagu aliteka Baghdad akamwua khalifa wa mwisho Al-Musta'sim Billah.
Mjomba wale Al Mustansir alifaulu kukimbia Misri alipoendelea kutumia cheo cha khalifa lakini bila mamlaka yoyote akiwa chini ya usimamizi wa watawala wa Misri waliojipamba na mwenye cheo hicho. Cheo kikaendelea kutumiwa hapa Misri kajini kwa jina tu hadi mnamo mwaka 1517 ambako Mwaabbasi wa mwisho mweye cheo hiki alipelekwa kwenda Konstantinopoli (Istanbul) kama mfungwa wa sultani wa Waosmani waliochukua cheo kutoka kwake.